Available via license: CC BY
Content may be subject to copyright.
43
Eastern Africa Journal of Kiswahili
Communication
Journal url: https://journals.editononline.com/
Uhalisia katika mashairi ya Kezilahabi (Dhifa)
Author
Jane Kanini Maithya
Email: maithyajk@gmail.com
[ISSN 2958-1036]
Volume: 01 Issue: 01 | Aug-2022
EAJK
Laikipia University, Kenya.
Cite this article in APA
Maithya, J. K. (2022). Uhalisia katika mashairi ya Kezilahabi (Dhifa). Eastern Africa journal of Kiswahili, 1(1), 43-49.
https://doi.org/10.51317/eajk.v4i1.183
Ikisiri
Fasihi ni kioo cha maisha. Humulika jinsi jamii ilivyo kwa kuangazia masuala
mbalimbali yanayoikumba. Waandishi wa kazi za fasihi huchota maudhui yao
kutokana na matukio mbalimbali yanayoikumba jamii, nia yao ikiwa ni
kuielimisha, kuiadilisha na kubeza maovu yanayotendeka. Makala hii
inaangazia uhalisia katika mashairi ya Diwani ya Dhifa iliyoandikwa na
Euphrase Kezilahabi (2008). Kupitia kwa mashairi yake, Kezilahabi ameichora
hali halisi iliyopo katika mataifa mengi ya Afrika kwa kumulika matatizo
mbalimbali yanayoyakumba. Anaupitisha ujumbe wake kwa kutoa taswira
nzito zinazoundwa kutokana na matumizi ya tamathali mbalimbali za usemi
ambazo zinaacha athari kubwa kwa wasomaji na kuwachochea kupata ari ya
kupigania haki za wanyoge. Utafiti huu unaongozwa na nadharia ya uhalisia,
ambayo kulingana na Wamitila 2002, iliwekewa msingi na mwanafalsafa
Hegel katika kitabu chake kinachojulikana kama Aesthetik. Utafiti
unawawezesha wanajamii hasa kutoka mataifa ya Kiafrika kuyabaini
matatizo mbalimbali wanayokumbana nayo na jinsi ya kujinasua kutokana na
minyororo ya umaskini.
Maneno muhimu: Uhalisia, tashihisi, tamathali za usemi.
A publication of Editon
Consortium Publishing (online)
Article history
Received: 10.07.2022
Accepted: 15.07.2022
Published: 15.08.2022
Scan this QR to read the paper online
Copyright: ©2022 by the author(s).
This article is an open access article
distributed under the license of the
Creative Commons Attribution (CC BY)
and their terms and conditions.
44
Eastern Africa Journal of Kiswahili
Communication
Journal url: https://journals.editononline.com/
UTANGULIZI
Diwani ya Dhifa iliandikwa na Euphrase Kezilahabi
(2008). Ni diwani iliyo na mashairi sitini ambayo yote
ni huru. Kezilahabi ni mwandishi mtajika sio tu katika
nyanja ya ushairi bali pia katika utanzu wa riwaya.
Katika diwani ya Dhifa, mshairi anataka wasomaji
wake wadadisi, wahoji, wachunguze na kuzichokonoa
nafsi zao, mazingira yao, siasa yao, nchi yao,
ujitambuzinafsi wao na hata maisha yao yenyewe
(Kezilahabi 2008). Mshairi anayazungumzia masuala
mengi yakiwepo utawala mbaya, ukoloni mamboleo,
umaskini na kifo. Hii ni diwani iliyokitwa kwenye
kupiga darubini falsafa nzima ya maisha ya binadamu
katika duara yake ya maisha yanayoanzia kwenye mji
wa mamake na kuishia kwenye mji wa kaburi.
Mtazamo wa Uhalisia
Mtazamo wa uhalisia humulika hali halisi ya jamii bila
kupunguza wala kuongeza chochote. Ni mtazamo
ambao Wafula na Njogu (2007) wanadai kuwa
muhimu zaidi kutokea katika karne ya kumi na tisa na
ishirini na pengine utaendelea kutuathiri katika karne
ya ishirini na moja. Wamitila (2002) anasema kuwa
dhana ya uhalisia hutumiwa kwa maana mbili kuu.
Kwanza, kuelezea tapo la kipindi maalum cha
kihistoria katika fasihi za Ulaya. Pili, kuelezea aina ya
mtazamo au tapo la kifasihi ambapo kazi za fasihi
zinachukuliwa kama zinazohifadhi au kuakisi sifa za
kimsingi zinazohusishwa na uhalisi. Kulingana naye,
kazi ambazo huangaliwa kama za kihalisia
zinatarajiwa kumulika hali halisi ya maisha katika jamii
husika. Anasema kuwa neno uhalisia huelezea kazi za
kifasihi ambazo huwakilisha ulimwengu wa maisha ya
kijamii ambako kuna wahusika au mhusika
anayetenda jambo kwa jinsi inayochochewa waziwazi
na hali iliyomo.
Kulingana na Wafula & Njogu (2007), uhalisia wa
kifasihi huashiria uwezo wa kusawiri au kuelezea hali
kwa kuzingatia uyakinifu au uhakika wa maisha.
Unahusu uigaji wa mazingira anamopatikana
binadamu. Mwandishi anayeongozwa na nadharia hii
hujibidiisha kuonyesha ukweli jinsi ulivyo na
kuonyesha picha kamili ya mazingira ambamo
mwanadamu anajipata. Wanasema kuwa mwandishi
anapaswa kuitoa picha ya jamii bila kuidunisha wala
kuipigia chuku. huweza kusuta maovu katika jamii
kwa kuwatetea watu fulani na kuwasuta wengine
kulingana na msimamo wake.
Wafula (1992) anasema uhalisia ulitokea kwa sababu
za kihistoria. Wachache wenye kumiliki njia za
kuzalisha mali walijibidiisha kujiimarisha huku
wakitumia nguvu za wanyonge. Wanyonge walichoka
na dhuluma kisha wakaungana kudai haki zao.
Msokile (1993) anasema kuwa nadharia hiyo ilianza
kupata nguvu wakati wa Eliot George wa Uingereza
na kufikia leo kuna aina nyingi za uhalisia kama vile
uhalisia wa kibwanyenye, uhalisia wa kijamaa na
uhalisia wa kiyakinifu. Kulingana naye, mwanahalisia
anastahili kushughulikia mambo yote bila kupuuza
jambo lolote katika jamii.
Momanyi (1991) ana maoni kuwa ikiwa fasihi itaweza
kuchukua jukumu la kusuluhisha matatizo yaletwayo
na mielekeo mipya katika jamii, jukumu ambalo
limesababishwa na historia, lazima kuwe na
waandishi wa kifalsafa na kisiasa ambao ndio huzaa
fasihi. Kezilahabi katika kuupitisha ujumbe wake kwa
wanajamii amezungumzia maudhui mbalimbali
ambayo yanatoa picha kamili ya matatizo mbalimbali
yanayowakumba watu katika mataifa mataifa ya
Afrika. Baadhi ya maudhui ni:
Ukoloni Mamboleo
Shairi la Dhifa limetungwa kumulika uongozi katika
Bara la Afrika. Kezilahabi anazungumzia wakati wa
ukoloni ambapo Wazungu na Waarabu
Waling’ang’ania na kuligawa Bara la Afrika kwa
manufaa yao wenyewe (Mbaabu, 1996). Dhifa ni
jazanda ya mkoloni kusherehekea baada ya kufaulu
kuzinyakua na kuzitawala nchi mbalimbali za Afrika.
Bwana Mkubwa katika shairi hilo ni taashira ya
viongozi wanaotawala kwa unafiki na kamasi ni
taswira inayoashiria uovu. Uovu unaozungumziwa ni
dhuluma dhidi ya watawaliwa, uonevu, ubaguzi wa
rangi, unyonyaji na unyang’anyi wa raslimali za umma.
Kimsingi, mfumo wa uongozi ulihakikisha kwamba
mataifa ya kikoloni yananufaika kwa vyovyote vile.
Mtunzi anasema, “Nzi atua pale na kulila kamasi.”
Anaashiria hali ya viongozi kufurahia matunda ya
uongo wao na kushabikia unafiki. Kezilahabi
anabainisha kuwa wanaonufaika kutokana na mfumo
huo ni mawaziri ambao hupata pesa nyingi, wabunge
45
Eastern Africa Journal of Kiswahili
Communication
Journal url: https://journals.editononline.com/
wanaopewa magari na waandishi wa habari, huku
maskini wakibaki nyuma bila kupata chochote.
Katika shairi la Njia Tulopitishwa, mtunzi anaashiria
athari za mfumo wa kikoloni wa ubepari. Anaeleza
kwamba mfumo wa kibepari umekita mizizi katika
jamii ya sasa. Anasema “Sasa wakokota tongotongo
nzito machoni kwa mswaki kuukuu.” Mswaki kuukuu
ni ishara ya mbinu ambazo zinatumika kuondoa athari
za mfumo wa kikoloni na ambazo hazina nguvu tena
ya kukabiliana na uozo uliopo katika jamii. Hata wale
wanaotegemewa kuleta mabadiliko ni zao la mfumo
huo. Kezilahabi anasema, “Kisha wanacheka gizani
kwa mawi yatokeayo.” Anamaanisha kuwa
wanaendesha mambo yao gizani kama vile ulaghai na
wanafurahia tendo hilo. Hata hivyo, ana matumaini
kuwa siku moja haki itatendeka.
Tamaa.
Nchi nyingi za Afrika zimeangamizwa na tamaa ya
viongozi. Rasilmali za nchi badala za kuwafaidi
wananchi zinawafaidi viongozi wachache. Shairi la
Madomo Mapana linaonyesha hali ya kusikitisha ya
wanyonge kutokana na kuwepo kwa viongozi ambao
wanajifikiria wao wenyewe bila kujali maslahi ya raia
na nchi wanazotawala. Raia wanateseka kutokana na
mfumo wa kibepari ambapo viongozi hudhibiti njia
zote za uzalishaji mali. Watawaliwa hunyonywa jasho
lao, hawafurahii matunda ya jasho lao wala uhuru
walioupata. Mtunzi anatumia tashbihi kuwachora
wanasiasa kama wezi wanaoiba mali ya umma bila
kujali kizazi cha kesho.
Katika shairi la Jibwa, mtunzi anaonyesha kuwa
viongozi wenye tamaa wakiwa uongozini tamaa yao
huongezeka na hawatosheki wala kujali utu na
maslahi ya wengine. Anaeleza kuwa jibwa likianza
kuiba huwa na mazoea ya kuendelea kuiba na huanza
na mayai (vitu vidogovidogo). Kezilahabi anasema,
“Kesho litakula kitovu cha mtoto wako pekee, jibwa
jizi fisi.” Kula kitovu cha mtoto ni sawa na kula kiini
cha maisha yake. Hii ina maana kuwa viongozi kama
hawa wanaweza kuangamiza chemichemi za maisha
ya walio wengi.
Shairi la Cha Watu limetumiwa kuwakashifu wazee
waliopigania uhuru ambao wana tamaa ya mali.
Mtunzi anasema, “Udenda wao umedondokea
chakula.” Anamaanisha kuwa kwa sababu ya tamaa
yao ya kupita kiasi, wamekula raslimali yote ya taifa.
Wameifilisi nchi na sasa wanajaribu hata mifupa.
Mtunzi anaashiria kuwa nchi nyingi za Afrika ziko
hatarini ya kuanguka kiuchumi kutokana na tamaa ya
viongozi.
Shairi la Jibwa limetumiwa kubeza tamaa ya viongozi
vilevile Mtunzi anasema:
Jibwa likishika hatamu
Haliwezi kuacha tamu
Litatumia kila hila
Litakacho likipate
Kezilahabi anasema kuwa dawa ya jibwa hilo ni shoka.
Anasema kuwa viongozi wenye tamaa hawawezi
kung’oka uongozini ila waangamizwe au wang’olewe
uongozini kwa nguvu.
Utabaka
Katika shairi la Dhifa, Kezilahabi anabainisha kuwa
wanaonufaika kutokana na mfumo wa ubepari ni
mawaziri ambao hupata pesa nyingi, wabunge
wanaopewa magari na waandishi waliopewa kazi.
Wazungu, Wahindi na Waarabu wanaitwa walanchi
kwa sababu pia hunufaika kutokana na mfumo wa
kidhalimu unaotawala nchi nyingi za Afrika. Mazingira
yanayoibua shairi hili ni mfumo wa utabaka usiojali
maslahi ya walio wengi. Katika shairi la Maendeleo si
Ndwele, mfumo wa kibepari unaoendelezwa ili
kuwakandamiza wanyonge katika jamii unamulikwa.
Tabaka tawala lilitumia mbinu na hila mbalimbali
kulinda na kudumisha maslahi yao kiuchumi. Azimio
lililenga kuleta usawa wa kiuchumi, kuondoa utabaka
na ubinafsi. Hata baada ya kutangazwa kwa Azimio,
kulikuwa na pingamizi kutoka kwa wale
walioendeleza mfumo wa ubepari. Mshairi anasema
‘Watoto wanagongana wao kwa wao’. Hapa
anamaanisha kuwa hata wale waliokuwa na mawazo
mazuri baada ya uhuru na azimio wameathiriwa na
mfumo wa kikoloni wa kupigania kipato.
Katika shairi la Ukweli Koko, mwandishi ametumia
kinaya anaposema, “Watawala wa Afrika ni wapenda
demokrasia, umaskini ni wa kujitakia.” Ukweli ni kuwa
watawala hao wanakiuka demokrasia ili kujilimbikizia
mali huku wananchi wakizama kwenye lindi la
umaskini. Shairi hilo linaonyesha jinsi utawala uliopo
umejaa unyonyaji na ukandamizaji. Ni uongo kuwa
46
Eastern Africa Journal of Kiswahili
Communication
Journal url: https://journals.editononline.com/
umaskini ni wa kujitakia na wafanyakazi ni wavivu.
Mfumo wa udhalilishaji ndio unaowaumiza na
kuwafanya walimao wasivune mazao ya jasho lao.
Kwa kusema kuwa ardhi, madini na nafaka ni mali ya
umma ni uongo kwa sababu ni mali ya walio
wachache au mali ya umma lakini kwa manufaa ya
walio wachache.
Shairi la Maskini linamulika udhalimu wa kitabaka
ambapo tabaka la juu linalidhulumu tabaka la chini.
Maskini wanaendelea kukandamizwa hadi kufa
kutokana na mfumo dhalimu usiojali watu wanaoishi
katika ulitima. Kazilahabi anasema, “Maskini
amechinja maelfu ya sisimizi, chajio cha mwisho.”
Maskini kutokana na kukosa chakula wanakula
wadudu na tunaambiwa ndicho chakula chao cha
mwisho kabla hawajakufa kutokana na njaa. Ni kinaya
kuwa maskini akifa, wanajamii wanamtupia majani
wasipatwe na laana ilhali walikuwa katika nafasi ya
kumwokoa lakini hawakumpa chakula.
Ukengeushi
Kukengeuka ni kudunisha mila na tamaduni za jamii
ya mtu na kufuata mila na tamaduni za jamii geni.
Kezilahabi anasema kuwa kukengeuka kwa Waafrika
kumechangia kuzorota kwa maendeleo hasa katika
nchi za Afrika. Shairi la Ukweli Koko limetumiwa
kuonyesha ya kwamba Kiingereza na Kifaransa ni
funguo za maisha. Hali hii inatokana na sababu
kwamba Waafrika hupuuza lugha zao za kienyeji na
kutukuza za kigeni wanazozihusisha na ustaarabu.
Kazelahabi ana maoni kuwa elimu ya kikoloni
hutumikia uchumi wa kibepari. Hali hii imemfanya
Mwafrika kuwa mtumwa katika mazingira yake. Kuwa
lugha za Afrika ni lugha za mtaani ni kuonyesha jinsi
tumezidharau lugha zetu za asili. Hii ni njia ya
kuendeleza ukoloni mamboleo.
Shairi la Mke wa Waziri linaonyesha jinsi binadamu
hujisahau hasa anapotoka katika tabaka la chini na
kuanza kuona walioshiriki naye kama watu duni.
Monika alibadilika alipofika mjini na kuolewa na
waziri. Tukio hili linamwathiri Monika kitabia,
kimtazamo na kimwenendo. Kezilahabi anasema:
Upitapo wainua kipua juu
chogo limechongoka kama senene
Aendaye kwenye harusi ya mende
Mtunzi anamsifu mwanamke anayeishi mashambani
ambaye licha ya kudunishwa na kuonekana mshamba,
hufanya kazi muhimu ya kulima na kupalilia mimea
ingawa wanaonufaika kutokana na jasho lake ni
matajiri.
Nafasi ya Vijana
Shairi la Marahaba linaonyesha haja ya watu
kujitambua na kujua kuwa yafaa waishi maisha adilifu
na kutumia nguvu zao kwa busara wakiwa vijana.
Anaonyesha kwamba watu wanavyozeeka ndivyo
matatatizo yao ya maisha yanavyoendelea
kuongezeka. Hii ina maana kwamba ni muhimu watu
kupanga maisha yao ya baadaye kama wangali wana
nguvu. Shairi hili linaonyesha kwamba vijana wana
nafasi muhimu katika jamii. Wana nguvu na
wanaweza kutekeleza mambo mengi.
Wimbo wa Unyago ni shairi linalowasisitizia vijana
kuishi maisha yao na wazee waishi yao. Ili vijana
waweze kuishi vizuri, wafaa kuepukana na ukabila.
Anawashauri wasichana waolewe kulingana na
mapenzi yao bali si kushurutishwa. Shairi la Cha Watu
linakashifu wazee waliopigania ukombozi kuchukulia
nchi kuwa ni yao. Wazee hao wamekatalia uongozini
huku vijana wakiambiwa wao ni viongozi wa kesho.
Wazee hao huwaona vijana kama watu wasio na
tajriba ya kuongoza.
Haki za Wafanyakazi
Shairi la Kwa Walimu Wote limetumiwa kuonyesha
dhiki zinazowakumba wafanyakazi wa serikali kama
vile walimu. Anachora taswira ya shida wanazopitia
walimu wakistaafu kama vile viatu vilivyoisha visigino,
sidiria chakavu na chupa tupu za pombe na marashi.
Umaskini huu unatokana na mshahara duni
wanaolipwa hivi kwamba hawawezi kujiwekea akiba
ya baadaye. Umaskini unamfanya mwalimu
kudharauliwa. Mtunzi anasema, “Nilipokuwa mwalimu
nikaitwa bure.” Hata hivyo, Kezilahabi anainua hadhi
ya mwalimu kwa kusema wana ushawishi mkubwa
kwa hivyo wanastahili kuwafunza watu kushirikiana
na kuachana na unafiki.
Shairi la Ukweli Koko linaonyesha jinsi jasho la
wakulima linawafaidi wengine. Wakulima wana
mateso mengi kwa sababu ya kunyanyaswa na
mfumo uliopo. Mfumo wa kibepari wenye ukiritimba
47
Eastern Africa Journal of Kiswahili
Communication
Journal url: https://journals.editononline.com/
unawanyonya wafanyakazi na kuwasingizia kuwa
wavivu. Mshairi ametumia kinaya kubeza viongozi wa
Afrika ambao ni wenye tamaa na ndio hunufaika
kutokana na jasho la wakulima huku wakidai ardhi na
fanaka ni mali ya umma. Shairi la Alalaye ni mfano wa
dhiki zinazowakumba wakulima na wavuvi. Mtunzi
anasema kuwa huku wakulima na wavuvi
wakiendelea kuumia, wale wanaofaa kuwaokoa
hawajali. Mtunzi anaposema mafuriko yaliyotokea
anaashiria hali inayoathiri masoko ya ulimwengu
ambayo hutangaza bei ya chini, jambo ambalo
huwapunja wakulima na wavuvi. Mtunzi anaendelea
kusema, “Tumeona mifupa ya kuku jalalani.” Kauli hii
inaashiria kwamba wakulima na wafugaji
wameshuhudia ishara kwamba kumekuwepo na
manufaa yanayotokana na jasho lao lakini
hawakushirikishwa katika uhondo huo. Hii ina maana
ya kwamba jasho lao linawafaidi wengine.
Ndoa
Katika shairi la Msamaha, Kezilahabi anaonyesha
umuhimu wa msamaha katika maendeleo ya jamii
hasa familia. Anaeleza kuhusu mhusika ambaye
ametambua makosa yake na sasa anaomba
msamaha. Kulingana na mtunzi, mhusika alimdhuru
mkewe na kumsababishia madhara makubwa Taswira
ya uso kuvimba inaashiria kwamba mume alimpiga
mkewe. Mume anakiri ya kwamba hakushawishiwa na
pombe wala hasira bali ni yeye mwenyewe. Hatua hii
inaonyesha uponyaji unaweza kupatikana katika ndoa
na jamii iwapo wanaohusika watatambua makosa
yao.
Katika shairi la Wimbo wa Unyango, mtunzi anashauri
wasichana waolewe kulingana na mapenzi yao bali si
kushurutishwa. Kezilahabi anawaambia vijana waoe
au kuolewa na wanaowataka bila kuzingatia ukabila.
Aidha, wasikubali kusikiliza umbea wa
wanaowaambia waume zao ni wabaya. Anasema
kuwa ili jamii ipate kuendelea, kuna umuhimu wa
kupanga uzazi. Wito ni kwamba watu wazae idadi ya
watoto ambao wataweza kuwalea huku wakitunza
afya zao kwa kuepuka kuzaa watoto wengi.
Mapinduzi na Ukombozi
Kezilahabi amezungumzia sana maudhui ya
mapinduzi na ukombozi. Katika shairi la Walimu Wote,
mtunzi anamhamasisha mwalimu kuwazindua
wanafunzi wake kuhusu haki zao badala ya kutunga
nyimbo za kuwasifu viongozi dhalimu. Vilevile,
anawahamasisha wananchi wote kwa jumla kuwa
ikiwa wangetaka mabadiliko, lazima waungane
pamoja na kupiga kura ili kuwaondoa viongozi
dhalimu mamlakani. Mtunzi anawaona walimu wana
nafasi muhimu kwa vile wana busara na wanaweza
kuuzindua umma kupitia kwa kuielimisha jamii.
Shairi la Madomo Mapana linaashiria kifo cha
wanasiasa dhalimu kitatoa suluhu kwa walio wengi
kupata afueni. Wananchi pia watajikomboa kutokana
na mfumo dhalimu. Mtunzi anasema:
Mwanasiasa afapo
Tumejikomboa na domo
Moja pana lizibwalo na mchanga
Katika shairi la Jibwa, mtunzi anasema ni muhimu
kupambana na viongozi wanaoendeleza hulka za
kikoloni ili kuwaangamiza kabisa. Hii ndio sababu
anasisitiza wito wa kulipiga jibwa kichwa, kulimwagia
petroli, kulifunga kamba shingoni na kuliburuzwa hadi
jalalani. Anasema ya kwamba huwezi kupigana nao
ana kwa ana. Ni muhimu kuwapangia mikakati ya
kuwaangamiza kisiasa kwa kupiga kura kwa busara ili
kuwaondoa uongozini. Katika shairi la Mafuriko,
mtunzi anawahamasisha wananchi kuhusu uchaguzi
bora wa viongozi. Anabainisha ya kwamba ni
kutokana na uchaguzi bora tu ambapo viongozi wa
zamani wataweza kuondolewa madarakani. Mafuriko
anayoyazungumzia mtunzi ni mapinguzi kupitia kwa
upigaji kura kwa busara ili kubadilidha viongozi
wanaoendeleza uongozi mbaya, jambo ambalo
litasababisha ujenzi wa jamii mpya hasa katika nchi za
Afrika. Wananchi watawachagua tu viongozi wenye
maono.
Uongozi Mbaya
Maudhui ya uongozi mbaya ambalo ndilo tatizo kuu
katika nchi nyingi za Afrika yamejadiliwa kwa kina
kupitia kwa mashairi mengi katika diwani ya Dhifa.
Shairi la Ulingoni linazungumzia mfumo wa uongozi
ambao haukubadilika hata baada ya uhuru. Licha ya
miaka mingi ya uhuru, hakuna chochote ambacho
kilionyesha matunda ya uhuru. Hata baada ya miaka
mingi ya uhuru, ukoloni mamboleo na ubepari ni vitu
ambavyo vilihitaji kushughulikiwa kwa kutumia mbinu
na mikakati mipya. Mtunzi anaonekana kutumia lugha
48
Eastern Africa Journal of Kiswahili
Communication
Journal url: https://journals.editononline.com/
kali ya matusi ili kuwabeza viongozi dhalimu
anaposema, “Wanacheza matako nje wala
hawapendezi. Na hakuna awashangiliaye. Wananchi
hawafurahii nyimbo zinazochezwa ulingoni kutokana
na dhuluma wanazofanyiwa na viongozi.
Shairi la Maendeleo si Ndwele linaonyesha jinsi
uongozi mbaya umesababisha umaskini katika Bara la
Afrika. Mtunzi anasema, “Baba atoka chumbani na
bunduki akiyumba. Hii inamaanisha kwa kukosa
mwelekeo, kiongozi wa taifa anatoka na kauli kali ya
kuangamiza maovu, lakini pia anayumbayumba kwa
kukosa msimamo thabiti. Inaamaanisha pia yeye
ameathirika. Kezilahabi anasema, “Akiimba wimbo wa
Taifa wa Afrika.” Anaashiria kuwa wao ni wamoja
katika taifa moja la Afrika.Wimbo huu ni ishara ya
unafiki kwa kuwadanganya watawaliwa kwamba
wako pamoja ilhali mipaka ya utabaka inandelea
kupanuka. Mshairi anasema, “Wimbo aliotunga akiwa
ndotoni.” Hapa anaashiria mambo mazuri anayowaza
tu lakini hatendi. Uongozi mbaya umesababisha
umaskini katika mataifa ya Afrika.
Shairi la Madomo Mapana linaangazia ulafi wa
viongozi ambao unafananishwa na zimwi ambalo
husukuma mtoto pembeni ili linyonye maziwa ya
mama yake. Kifo cha viongozi hao ni furaha kwa
wananchi kwa vile hawana umuhimu ila kuifilisi nchi.
Mtunzi anawaona walimu ndio wenye busara na ndio
wanapaswa kuiongoza nchi kwa sababu hao ndio
huona mbali. Anasema:
Nchi mmeifilisi waachieni walimu
Wakajenge taifa jipya
Kama hamwezi kuona mbele
Katika shairi la Dhifa, Kezilahabi anawaita Wazungu,
Wahindi na Waarabu walanchi kutokana na tabia yao
ya kulipora Bara la Afrika. Mawaziri na Wabunge
wanakula na kuishi maisha ya kifahari huku maskini
wakiteseka. Viongozi hao wanalinganishwa na nzi
wanaokunya kutokana na shibe huku maskini
wakiangamizwa na njaa. Mtunzi anawafananisha
viongozi hao na zimwi ambalo limemeza watoto wote
kijijini katika shairi la Zimwi. Taswira hiyo imetumiwa
kuonyesha jinsi viongozi fisadi huangamiza maisha ya
kesho ya watoto wetu kutokana na tamaa na ufisadi.
Wanakijiji wanalifuata wakitaka kuliangamiza huku
wakiongopa hatari iliyopo kwa vile zimwi lina nguvu.
Viongozi hao wanaogopwa na wananchi kwa sababu
wamelindwa na vyombo vya dola. Ni mazimwi
ambayo ingawa yanatujua yanatula na kutumaliza.
Dhuluma
Katika shairi la Makaburini, Kezilahabi anaeleza
masaibu yanayowakumba watoto yatima. Msichana
husingiziwa umalaya na mvulana kuambiwa ya
kwamba ameambaa tabia ya ulevi kama babake. Ni
bayana kwamba mayatima wanateseka sana
mikononi mwa jamaa zao wanaofaa kuwalinda.
Watoto hao wanateseka kwa kufanywa wafanyakazi
wa kazi duni kama vile kuuza kwa baa badala ya
kupelekwa shuleni wapate elimu. Shairi la Hoja
linadhihirisha kuwa unyanyasaji umekithiri katika
jamii. Watu hawajali hisia za wenzao. Mtunzi
anatuchorea taswira ya namna wanyonge
wanavyoangamizwa. Ni kinaya kwamba maovu kama
vile ubakaji, unyanyasaji na uonevu hasa kwa
wanyonge yanaendelea na hakuna anayejali.
Nafasi ya Mwanamke
Katika shairi la Binti, mtunzi amemchora mwanamke
kama kiumbe duni ambaye kazi yake ni kuwafurahisha
wanaume. Anamsihi akatae kuwa ubao wa matangazo
au vilabu vya mpira. anamhamasisha mwanamke
ajihisi huru na atende yanayomridhisha. Anamshauri
kupigania haki zake katika jamii inayomsawiri kama
kiumbe duni na apate elimu itakayomsaidia kujinasua
kutokana na minyororo ya utumwa. Mtunzi katika
Shairi la Hoja anabeza ubabedume unaoendelezwa na
jamii dhidi ya mwanamke. Analinganisha kisa
alichokisoma cha kijana akimbaka msichana wa miaka
kumi na sita na simba anayemfukuza pundamilia.
Anasema dhuluma ya ubabe inaweza kuharibu umma.
Umaskini
Kezilahabi amezungumzia maudhui ya umaskini kwa
kina katika shairi la maskini. Maskini hupuuzwa na
kuonekana kuwa watu wasio muhimu. Katika shairi
hili, maskini anasema kuwa ananongwa na njaa na
amekondeana kama siafu. Hakuna anayesikia kilio
chake cha mateso. Matajiri wameweka nta kwenye
masikio yao ili wasisikie kilio cha wanyonge. Licha ya
kuwa nchi yenyewe ni tajiri, wanaonufaika ni matajiri
huku maskini wakila makombo yaliyobaki.
Nikinywa maji ya mvua
Yaliobaki juu ya jani la mti
49
Eastern Africa Journal of Kiswahili
Communication
Journal url: https://journals.editononline.com/
Wa utajiri utiririkao kama mto.
Shairi la Kwa Walimu Wote linaonyesha kuwa licha ya
walimu kutoa mchango mkubwa katika jamii,
wanapostaafu huishi maisha ya uchochole.
Kumbuka mwalimu utakapostaafu
Mijusi watataga mayai ndani ya viatu
Vyako vilivyoisha visigino
Mende watazaliana ndani ya chupa tupu
Za marashi na bia
Hali hiyo inatokana na mshahara duni wanaolipwa
walimu ambao hauwezi kuwawezesha kuweka akiba
ili wawe na maisha mazuri ya baadaye.
Katika shairi la Maskini 11, mtunzi anasema maskini
anakula chakula chake cha mwisho ambacho ni
sisimizi. Kula sisimizi kunatokana na kukosa chakula
bora cha kula kutokana na umaskini. Anapokufa kwa
njaa, hakuna anayeathiriwana na kifo chake. Wapita
njia hawajali wanamwona alikufa kutokana na laana
ya kuwa maskini.
Kifo
Katika shairi la Wazo Nje ya Wakati, mtunzi anatumia
mbinu ya tashihisi kuonyesha kuwa kifo hakina
huruma. Anasema kuwa kifo hufurahia watu
wanapopatwa na magonjwa kama kansa, magari
yanapogongana, ndege zinapoanguka na
kunapotokea vita. Mtunzi anakiita kifo wazo nje ya
wakati, kumaanisha ni kitu kisichoeleweka na
kutabirika. Anatufahamisha kuwa lazima kila
mwanadamu atakufa kwa hivyo hamna haja ya
kuogopa kifo. Shairi la Makaburini linamulika matatizo
wanayoyapitia watoto mayatima baada ya vifo vya
wazazi wao. Watoto hao huonekana kuwa mzigo na
walezi wao. Chochote kinachopotea huambiwa wao
ndio wameimba. Wavulana huitwa wezi kama baba
zao na wasichana malaya kama mama zao. Hunyimwa
elimu huku jamaa za wazazi wao waking’ang’ania
ardhi ya wazazi wao. Kazi yao huwa ni kuwauzia
wateja bar iliyokuwa ya wazazi wao. Katika shairi la
Mahojiano na Kifo, Kezilahabi anajibizana na kifo
akikiambia hakina hisia. Anasema kuwa kifo hakibagui
matajiri wala maskini, vijana na wazee. Kifo hakina
jibu lolote kwa sababu shutuma zote zinazoelekezwa
kwake ni za kweli. Shairi la Marahaba linaeleza hali ya
watu kujitambua na kujua kuwa yafaa waishi maisha
adilifu. Mtunzi anatuhimiza kuelewa hapa duniani sisi
ni wasafiri. Maisha yetu ni mafupi kwa hivyo tujue
namna ya kuishi. Tukiishi vyema, hatima yetu pia
itakuwa njema. Mtunzi anaonyesha kuwa maisha ya
sasa yana changamoto nyingi. Changamoto hizi
zimechangiwa na usasa ambao umewafanya
wanajamii kugongana. Kwa mujibu wa mtunzi
miongoni mwa mambo yanayotokana na usasa ni
utovu wa maadili.
MAHITIMISHO
Makala hii inamulika maudhui mbalimbali
anayoyaeleza Kezilahabi katika diwani yake ya Dhifa.
Anazungumzia masuala mbalimbali yanayoiathiri jamii
katika mataifa mengi ya Afrika. Baadhi yao ni
umaskini, uongozi mbaya, dhuluma, matatizo
anayozikumba ndoa na mengineyo. Nia yake ni
kuwachochea wanajamii watafakari kuhusu hali
inayowakumba na wapate ari ya kujinasua kutoka
kwenye minyororo ya maonevu.
MAREJELEO
Kezilahabi, E. (2008). Dhifa. Nairobi: Vide-Muwa Daisy Publishers Limited.
Mbaabu, I. (1996). Language Policy in East Afrika: A Dependency Theory Perspective. Educational Research and
Publications.
Momanyi, C. (1991). Taswira kama Kielelezo cha Uhalisi katika Utenzi wa Al-inkishafi. Unpublihed M.A Thesis,
Kenyatta University.
Msokile M. (1993). Misingi ya Uhakiki wa Fasihi. Nairobi: East African Educational Publishers Limited.
Wafula R. M. & Njogu K. (2007). Nadharia ya Uhakiki wa Fasihi. Nairobi: The Jomo Kenyatta Foundation.
Wafula, R. M. (1992). Nadharia kama Mwongozo wa Utunzi na Uhakiki, Makala ya Semina, Chuo Kikuu cha
Nairobi.
Wamitila, K. W. (2002). Uhakiki wa Fasihi, Misingi na Vipengele Vyake. Nairobi: Phoenix Publishers Ltd.